Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameipongeza Wizara ya Maji inayoongozwa na Mhe. Jumaa Aweso pamoja na Wataalamu wa Wizara hiyo kwa matumizi mazuri ya Fedha za miradi katika utekelezaji na usimamizi mzuri wa miradi wa maji kote nchini,na kuagiza iwe mfano katika miradi mingine yote ya serikali.

Mhe. Rais ametoa Pengezi hizo kwa Mhe.  Waziri wa Maji na Wataalamu wa Wizara hiyo baada ya kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi ya maji nchini, ikiwemo utekelezaji wa Mradi Mkubwa wa Maji wa chanzo cha Ziwa Victoria aliyouzindua leo Oktoba 17,2023 katika Kijiji cha Kisonzo, Shelui-Singida.

Aidha,Mhe. Rais ameiagiza Wizara ya Maji kuongeza kasi katika usambazaji wa maji kwa wananchi, kwani amefarijika kuona suala la maji linafanyiwa kazi na serikali na maji yanapatikana tofauti na awali alipokuwa anapokelewa kwenye ziara zake na ndoo na chupa za maji wananchi wakielezea tatizo la maji, hali ambayo haipo tena.

Katika kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maji, Mhe. Rais ameziagiza Mamlaka zinazohusika kuhakikisha hapatokei mkwamo kwa sababu zozote katika upatikanaji wa misamaha ya kodi inayostahili,ucheleweshaji wa vibali vya kazi kwa wafanyakazi wa kigeni na utoaji wa vifaa bandarini.