Mahali Skimu ya Maji wa Ziwa Victoria ipo kijiji cha Ihelele, Wilaya ya Misungwi, takribani km 120 Kaskazini - Magharibi mwa Mji wa Shinyanga na km 110 Kusini - Magharibi mwa Jiji la Mwanza.
Choteo na Kituo cha Uzalishaji Maji Skimu ya Maji wa Ziwa Victoria inajumuisha choteo la maji, matangi ya kutuamisha tope, chujio za maji, mfumo wa kutibu maji, pampu kubwa za kusukuma maji kuelekea kwenye tangi kubwa la kuhifadhia maji na mabomba makubwa ya kusafirishia maji kuelekea kwa wateja. Choteo la maji limejengwa kwenye ukingo wa Ziwa Victoria katika Kijiji cha Ihelele; umbali wa takriban km 3.3 kutoka kwenye mtambo wa kuchuja na kutibu maji.
Choteo la maji kutoka ziwani kupeleka kwenye pampu
Kutibu na Kuhifadhi Maji Kutoka kwenye choteo hilo, majighafi husukumwa kwa pampu kupitia bomba la chuma lenye kipenyo cha mm 900 hadi kwenye mtambo wa kuchuja na kutibu maji, ambapo maji hupitia hatua kuu tatu. Hatua hizo ni utuamishaji tope, uchujaji na uuaji wa vimelea vinavyosababisha magonjwa. Baada ya hatua hizo, maji huwa tayari kwa ajili ya matumizi na husukumwa kwa pampu kubwa kupitia bomba la chuma lenye kipenyo cha mm 900 hadi kwenye tangi kubwa lililojengwa kileleni mwa Mlima Mabale, likiwa umbali wa takriban km 6.6. Tangi hilo lina uwezo wa kuhifadhi maji kiasi cha lita milioni thelathini na tano (35,000,000).
Tangi kubwa la Mabale lenye uwezo wa kuhifadhi lita 35,000,000.
Kituo cha Uzalishaji Maji Ihelele
Usambazaji Kutoka kwenye tangi la Mabale, maji hutiririka kwa mserereko kuelekea kwa wateja wa Mijini na Vijijini katika Mikoa ya Shinyanga na Mwanza. Mtandao wa usafirishaji maji unajumuisha mabomba makubwa ya chuma yenye jumla ya urefu wa takriban km 378 na kipenyo kuanzia inchi 48 (mm 1,200) kwenye tangi la Mabale hadi inchi 8 (mm 200) kwenye matangi madogo ya Vijijini. Kituo cha kuzalisha maji Ihelele kina maabara yenye vifaa kwa ajili ya kupima ubora wa maji kabla na baada ya kuzalishwa. Aidha, kwenye Miji ya Shinyanga na Kahama kuna vituo vidogo vya kuongeza kiwango cha dawa ya kuua vimelea vinavyosababisha magonjwa (chlorine gas). .
|