Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama Shinyanga (KASHWASA) Eng. Patrick Nzamba leo tarehe 17/05/2022 amefanya ukaguzi kwenye ujenzi wa Tanki la maji unaoendelea kwenye Mji wa Mwakitolyo (Shinyanga DC).

Katika ziara hiyo, Mkurugenzi Nzamba ameridhishwa na ubora pamoja na kasi ya ujenzi wa Tanki hilo unaofanya na Mkandarasi aitwaye Renatus Mbaruku. Hatahivyo Eng. Nzamba amemtaka Mkandarasi huyo aharakishe kumalizia sehemu ya kazi iliyosalia pamoja na kuyafanyia kazi mapungufu yote aliyoyabaini ili huduma zianze kutolewa haraka.

Aidha, Eng. Nzamba ametoa maagizo kadhaa kwa Mkandarasi huyo. Miongoni mwa maagizo hayo ni pamoja na kumtaka mkandarasi huyo azingatie suala la usalama kazini kwa kuhakikisha kwamba wafanyakazi wake wote wanavaa vifaa vya usalama kazini pamoja na kuweka sanduku la huduma ya kwanza (first Aid Kit).

Ujenzi wa Tanki hili la maji ni muendelezo wa jitihada zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita za kuhakikisha kwamba huduma ya maji inamfikia kila mwananchi. Gharama za ujenzi wa mradi huu ni Tsh 367,034,500/=, fedha zote zimetolewa na Serikali ya awamu ya sita kupitia Wizara ya Maji.