Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama Shinyanga (KASHWASA) na Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Shinyanga leo tarehe 1/12/2020 wamekutana na kutoa elimu mbalimbali kwa Jumuiya za huduma ya maji Mkoa wa Shinyanga.

 

Jumuiko hilo limefanyika kwenye ukumbi wa Shy Park Hotel mjini Shinyanga na kuhudhuriwa na Jumuiya zote za huduma ya maji Mkoa wa Shinyanga pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya maji.

 

Katika jumuiko hilo, KASHWASA iliwakilishwa na Ndugu John Zengo ambaye alitoa Salam za KASHWASA kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji.

 

Pamoja na Mambo mengine, Ndugu Zengo aliwaelezea washiriki wa jumuiko hilo mafanikio mbalimbali ambayo KASHWASA imekuwa ikiyapata tangu ianzishwe mwaka 2009 ikiwemo ukamilishwaji wa miradi mbalimbali ya maji.

 

Pia aliwaelezea washiriki hao kuhusu ushirikiano mzuri uliopo kati ya KASHWASA na Jumuiya hizo za huduma ya maji Mkoa wa Shinyanga. Amesema kwamba, Jumuiya hizo za huduma ya maji zimekuwa zikitoa ushirikiano wa karibu sana kwa KASHWASA ikiwemo kuwa mabalozi wazuri wa kutoa taarifa mbalimbali zinazohusu changamoto ya miundombinu ya KASHWASA pamoja na hujuma ya miundombinu hiyo.

 

Aidha Ndugu Zengo amewarai washiriki hao kuendelea kushirikiana na KASHWASA ili kuhakikisha kwamba wananchi wanaendelea kupata huduma ya maji Safi na salama.

 

Vilevile Ndugu Zengo amewakumbusha washiriki hao kuhusu kuanza rasmi kwa bei mpya ya maji kuanzia mwezi ujao wa Januari, 2021.

 

Ndugu Zengo pia amepongeza Mahusiano mazuri yaliyopo kati ya KASHWASA na RUWASA Mkoa wa Shinyanga, zikiwemo Wilaya zake zote.

 

Ameongeza kwamba Mahusiano hayo mazuri ni lazima yalindwe na yadumishwe na pande zote mbili.

 

Kikao hiki cha kukutana na Jumuiya hizo za huduma ya maji pamoja na wadau ni zao la mojawapo ya maazimio yaliyofikiwa hivi karibuni kwenye kikao cha pamoja kati ya KASHWASA na RUWASA kikao ambacho kiliongozwa na watendaji wakuu wa RUWASA na KASHWASA ambao ni Eng. Clement Kivegalo (Mtendaji Mkuu- RUWASA) na Eng. Joshua Mgeyekwa (Mkurugenzi Mtendaji wa KASHWASA).