Shughuli za uchimbaji wa madini usiofuata kanuni na taratibu zilizowekwa na Serikali unachangia kwa kiasi kikubwa kwenye uchafuzi wa vyanzo vya maji.

Mradi mkubwa wa maji kutoka ziwa Victoria ni miongoni mwa wahanga wa tatizo hilo.

Imebainika kuwa shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu usiofuata kanuni na taratibu kwa baadhi ya wachimbaji wa Mgodi wa Dhahabu wa Mwakitolyo umekuwa miongoni mwa vyanzo vikubwa vya uchafuzi wa chanzo cha Maji cha Ihelele.

Hayo yamebainishwa hivi karibuni na timu ya Maafisa kutoka Wizara ya Maji pamoja na KASHWASA waliokwenda kuona jinsi shughuli za uchimbaji wa madini unavyofanywa kwenye Mgodi wa Dhahabu wa Mwakitolyo.

Katika ziara hiyo, ilibainika kuwa chemikali zinazotumika kwenye uchenjuaji wa madini kwenye eneo hilo la Mwakitolyo zinauwezekano mkubwa wa kutiririka hadi kwenye mkondo wa chanzo cha Maji cha Ihelele.

Ili kukabiliana na tatizo hili, ujumbe huo wa Maafisa kutoka Wizara ya Maji pamoja na KASHWASA uliazimia kuwa pawepo na utoaji endelevu wa elimu kwa wachimbaji hao ili kunusuru ongezeko la uchafuzi wa chanzo cha Maji cha Ihelele pamoja na Mazingira.

Ziara hiyo ya Maafisa kutoka Wizara ya Maji pamoja na KASHWASA iliongozwa na Eng. Laurence Wasala ambaye pia ni Meneja Ufundi kutoka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama Shinyanga (KASHWASA) ambaye alikuwa Mwenyekiti wa ujumbe huo.