Wakuu wa Wilaya katika Mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Tabora wamepokea msaada wa Mapipa kutoka Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Kahama Shinyanga (KASHWASA).

Wakizungumza nyakati tofauti, Wakuu hao wa Wilaya wameishukuru KASHWASA kwa msaada huo wa Mapipa ambayo wamesema ni mchango mkubwa sana kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona katika Wilaya zao hususani kwenye maeneo yanayotoa huduma za kijamii kama vile masoko, stendi za mabasi na kwenye minada.

Akikabidhi Mapipa hayo kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi, Mkurugenzi Mtendaji wa KASHWASA Mhandisi Joshua Mgeyekwa amewaambia Wakuu hao wa Wilaya kwamba msaada huo unalengo la kuunga mkono juhudi za Serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona. Hadi sasa, jumla ya Mapipa 105 yenye ujazo wa lita 22,050 yamekabidhiwa kwenye Wilaya za Misungwi, Kwimba, Shinyanga Vijijini, Nzega, Igunga, na Uyui huku Wilaya za Kishapu na Kahama zikiwa zinasubiri awamu ya pili ya usambazaji wa Mapipa hayo.

Wakati huo huo, Mji wa Igunga Mkoani Tabora umeungana na Mji wa Nzega kwa kuanza kupata huduma ya maji toka Ziwa Victoria unaosimamiwa na KASHWASA mapema wiki jana. Kuanza kwa huduma hii ya maji kumetokana na kukamilika kwa taratibu zote za kiutendaji kati ya Mamlaka za Maji Igunga (IGUWASA) na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama Shinyanga (KASHWASA). Taratibu hizo za kiutendaji zilifanyika tarehe 30/4/2020 katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Igunga

Picha ya kwanza kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Mheshimiwa Juma Sweda akipokea msaada wa Mapipa toka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa KASHWASA Mhandisi Joshua Mgeyekwa. Wengine wakipokea msaada huo ni Muwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Ndugu Kulwa John (picha ya pili kutoka kushoto), Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mheshimiwa Jasinta Mboneko (picha ya tatu kutoka kushoto), Mkuu wa Wilaya ya Nzega Mheshimiwa Godfrey Ngupula (picha ya nne), Mkuu wa Wilaya ya Igunga Mheshimiwa John Mwaipopo (picha ya tano kutoka kushoto), na picha ya mwisho ni Mkuu wa Wilaya ya Uyui Mheshimiwa Gift Isaya Msuya.