Mji wa Nzega umekuwa wa kwanza Mkoani Tabora kuanza kunufaika na mradi wa maji toka ziwa Victoria ulio katika hatua za mwisho za ujenzi baada ya huduma hii kuanza kutolewa kwa wateja rasmi hapo jana tarehe 23/4/2020.

Kuanza kwa huduma hii ya maji kumetokana na kukamilika kwa taratibu zote za kiutendaji kati ya Mamlaka za Maji Nzega (NZUWASA) na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama Shinyanga (KASHWASA).

Taratibu hizo za kiutendaji zimekamilishwa kwenye ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Nzega na watendaji wakuu wa Mamlaka hizo huku Bodi ya Wakurugenzi ya KASHWASA ikiwakilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo Mhandisi Joshua Mgeyekwa na ile ya Nzega ikiwakilishwa na Mhandisi Lightness Gai.

Akizungumza kwa niaba ya Serikali, Mkuu wa Wilaya ya Nzega Mheshimiwa Godfrey Ngupula ameipongeza serikali ya awamu ya tano kwa kuwafikishia wananchi wake huduma hiyo muhimu ya maji ambayo wamekuwa wakiisubiri kwa muda
mrefu. Aidha, Mkuu wa Wilaya amebainisha kwamba kufika kwa huduma ya maji toka Ziwa Victoria Wilayani kwake ni fursa kubwa ambayo amesema itachochea maendeleo ya haraka kwa wananchi wake.

Akizitaja baadhi ya fursa hizo, Mkuu wa Wilaya amesema wananchi wake sasa wataweza kuanza kuyatumia maji hayo kwenye shughuli zao za viwanda, kuanzisha bustani, gharama za ujenzi kushuka, pamoja na fursa zingine zinazohusiana na huduma ya maji.

Mkuu wa Wilaya ameahidi kuwa Serikali wilayani Nzega itatoa ushirikiano wa hali ya juu kuhakikisha kwamba huduma hii haikwamishwi na inakuwa endelevu. Aidha, amewaomba wananchi watakaounganishiwa maji hayo wawe wanalipia ankara zao kwa wakati. Pia amewaelekeza Mamlaka ya maji Nzega (NZUWASA) kuwa wakali kwa mteja yoyote atakayekuwa mzembe kulipia ankara yake, ameongeza kwamba mteja yoyote (ikiwemo ofisi yake) atakayekuwa halipii ankara yake kwa wakati akatiwe maji bila kujali nafasi yake.