Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama Shinyanga (KASHWASA) imekutana na wadau wake siku ya Jumatatu tarehe 20/4/2020 kwenye ukumbi wa mikutano wa Mamlaka hiyo mjini Shinyanga.

Kikao hicho kilifunguliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa KASHWASA Mhandisi Joshua Mgeyekwa. Akifungua kikao hicho, Mhandisi Mgeyekwa aliwaeleza wajumbe hao kuwa lengo la kikao hicho ni kujadili Mkataba wa Huduma kwa Mteja.

Aliwaeleza kwamba Mkataba huo ni makubaliano kati ya KASHWASA na Wateja pamoja na wadau wao hivyo wanahusika moja kwa moja kuupitia Mkataba huo na kutoa maoni, mapendekezo, au maboresho. Mkurugenzi alifafanua kwamba Mkataba huo unahusu pande mbili hivyo ni lazima wao kama wateja na wadau kushiriki katika uandaaji wa makubaliano yaliyomo kwenye Mkataba huo.

Mwisho, Mkurugenzi aliwaeleza wajumbe kwamba Mkataba huo ni takwa la Kisheria ambalo linawataka watoa huduma wote nchini wakiwemo KASHWASA kuwa na Mkataba wa huduma kwa Mteja ambao lazima ujadiliwe na kukubalika na wateja.
Wadau hao walipata fursa ya kuujadili Mkataba huo pamoja na kutoa maoni na mapendekezo yao ambayo yote yalikubaliwa na Manejimenti ya KASHWASA.

Miongoni mwa wateja na wadau waliohudhuria kwenye kikao hicho ni pamoja na Mgodi wa Almasi wa Mwadui, Mamlaka za Majisafi wa Mazingira Kahama (KUWASA), Mwanza (MWAUWASA), Kishapu (KIWASA), pamoja na Jumuiya za watumia maji kutoka Shilabela, Mwamashimba, Iselamagazi, Unyanyembe, Mwagiwa, Bunambiyu, na Ikonongo.