Serikali imekiri kulidhishwa na miradi yote ya maji inayosimamiwa na KASHWASA. Hayo yamesemwa siku ya Ijumaa tarehe 17/4/2020 na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maji na Usafi wa Mazingira toka Wizara ya Maji na Umwagiliaji nchini Mhandisi William Christian alipofanya mahojiano mafupi na mwandishi wa taarifa hizi huko Ihelele, Misungwi.

Mhandisi Christian ameongoza ujumbe toka Wizara ya Maji na Umwagiliaji nchini ambapo pamoja na sehemu zingine, Ujumbe huo umetembelea ofisi ya KASHWASA mjini Shinyanga na kufanya mazungumzo na Menejimenti ya Mamlaka hiyo.

Akizungumzia miradi ya maji, Mhandisi Christian amesema kwamba, katika maeneo yote aliyokagua yeye pamoja na ujumbe wake, wamelidhishwa na huduma inayotolewa na KASHWASA ikiwemo utunzaji wa miundombinu ya maji katika maeneo nayo. Ameyataja baadhi ya maeneo waliyoyakagua kuwa ni pamoja na Igunga, Nzega, Shinyanga, Solwa, na kwenye chanzo cha maji huko Ihelele Wilayani Misungwi.

Aidha, Mhandisi Christian ameipongeza KASHWASA kwa kusudio lake la kuanza kutoa rasmi huduma ya maji muda wowote kuanzia sasa katika miji ya Nzega na Igunga, pamoja na Jumuiya za Watumia Maji katika maeneo hayo.

Mwisho, Mhandisi Christian ametoa rai kwa manejimenti ya KASHWASA kuanza kujipanga kwa ajili ya kuanza kutoa huduma ya maji kwa mji wa Tabora. Katika ujumbe huo, wajumbe waliofuatana na Mhandisi Christian ni pamoja na Ndugu Simoni Nkanyemka (Mkurugenzi idara ya huduma za Sheria), Dr. C.P. Nditi (Mkurugenzi Idara ya Ununuzi wa Umma), Mhandisi Edward Mulumba (Mhandisi Mkuu Wizara ya Maji), Ndugu Barnabas Ndunguru (Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu) na Mhandisi Edward Tindwa ambaye ni Mhandisi Msaidizi na Mratibu wa Mradi wa Maji Nzega, Igunga, na Tabora.