Mkurugenzi Mtendaji wa KASHWASA Mhandisi Joshua Mgeyekwa mwanzoni mwa wiki hii ameongoza mazungumzo ya mkakatikazi yaliyowaleta pamoja viongozi wa Mamlaka za Maji Kahama KUWASA na KASHWASA. Mazungumzo hayo yamefanyika siku ya jumatatu tarehe 5/4/2020 katika ukumbi wa mikutano wa KUWASA mjini Kahama.

Katika mazungumzo hayo, Mhandisi Mgeyekwa aliupongeza uongozi wa KUWASA kwa kuendelea kushirikiana na KASHWASA katika utoaji huduma bora kwa wateja wake. Aidha, Mhandisi Mgeyekwa alifurahishwa na mawasiliano ya mara kwa mara kati ya mamlaka hizi mbili kwani yamerahisisha upashanaji wa habari na taarifa zote muhimu kati ya mamlaka hizi. Mhandisi Mgeyekwa ameongeza kwamba upashanaji wa taarifa wa mara kwa mara kati ya mamlaka hizi siyo tu kwamba yamesaidia kushirikishana baadhi ya taarifa zinazozihusu mamlaka hizi bali pia yamesaidia kuendelea kuimarisha mahusiano mazuri yaliyopo kati ya mamlaka hizi pamoja na wateja wake.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa KUWASA Ndugu Allen Marwa kwa niaba ya wafanyakazi wa KUWASA alisema kwamba amefurahishwa kwa kutembelewa na uongozi wa KASHWASA ofisini kwake. Aidha, Ndugu Marwa amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa KASHWASA Mhandisi Mgeyekwa na ujumbe wake kwa kuamua kuwatembelea.

Hii siyo mara ya kwanza kwa uongozi wa KASHWASA kufanya ziara za aina hii kwa wateja wake kwani kumekuwepo na ziara za mara kwa mara za kuwatembelea wateja wake ambayo nia kubwa imekuwa ni kuendelea kuimarisha mahusiano mazuri yaliyopo kati ya mamlaka na wateja wake wote.