BODI YA ZABUNI KASHWASA YAKOSHWA NA UJENZI WA MRADI WA MAJI WA MIJI YA SIKONGE,KALIUA NA URAMBO- TABORA.

Bodi ya Zabuni ya KASHWASA imekoshwa na utekelezwaji wa ujenzi wa mradi wa maji ya Ziwa Viktoria kutoka Tabora kwenda Miji ya Sikonge, Urambo na Kaliua Mkoani Tabora.

Akizungumza leo tarehe 7 Novemba 2024 akiwa ziarani kutenbelea mradi huo, Mwenyekiti wa Bodi hiyo ya Zabuni Eng. Felician Kabigumila anasema kwamba kazi inayofanywa na Mkandarasi Megha Engineering ni nzuri na inafanywa kwa weledi na kiwango cha hali ya juu.

Eng. Kabigumila anasema kwamba utendaji kazi wa Mkandarasi ni wa kuigwa kwani anafanyakazi kwa kuzingatia viwango na muda uliopangwa kutekelezwa kwa ujenzi wa mradi huo.

Akitoa taarifa kuhusu ujenzi wa mradi huo, msimamizi wa mradi huo Eng. Bety Kaduma ameiambia Bodi hiyo ya Zabuni kwamba hadi sasa ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 50 kwa ujumla ambapo kwa mji wa Sikonge upo asilimia 55 na kwa Kaliua na Urambo upo asilimia 45. Anaongeza kwamba kulingana na mkataba wa ujenzi wa mradi huo, hadi sasa Mkandarasi yupo kwenye hatua nzuri ya utekelezaji ukilinganisha na muda alioanza ujenzi wa mradi huo.

Ujenzi wa mradi huo wenye gharama ya zaidi ya shilingi Billion 143.26 ulianza tarehe 11/04/2023 na unatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 10/04/2025. Kukamilika kwa mradi huo kutaiongezea KASHWASA eneo la utoaji wa huduma ya maji na unatarajia kuhudumia wananchi zaidi ya 490,00 kwenye Miji hiyo ya Sikonge, Urambo na Kaliua Mkoani Tabora.