WAZIRI WA MAJI MHE. JUMAA AWESO ASEMA HAKUNA KADA KUBWA WALA NDOGO NDANI YA WIZARA YA MAJI

Waziri wa maji Mhe. Jumaa Aweso anasema kwamba ndani ya wizara ya maji hakuna kada yenye hadhi kubwa wala ndogo kuliko nyingine ndani ya wizara ya maji.

Mhe. Aweso ameyasema hayo leo tarehe 14 Novemba, 2024 kwenye Ukumbi wa NSSF Ilala jijini Dar es Salaam alipokuwa anafungua kikao cha Maafisa Habari na Uhusiano, Maafisa Utumishi na Rasilimali Watu, pamoja na Maafisa Maendeleo ya Jamii wa wizara ya maji na Taasisi zilizopo chini ya wizara ya maji.

Mhe. Aweso anafafanua kwamba kuna baadhi ya kada ndani ya wizara ya maji ambazo zinajiona ni bora kuliko kada zingine zote. Anasema kwamba dhana hii siyo sahihi na haiungi mkono.

Mhe. Aweso anaeleza kwamba kada zote zilizomo kwenye wizara ya maji na Taasisi zake hazikuwekwa kimakosa kwani kila kada inakazi zake na mchango wake chanya kwenye shughuli na mafanikio ya wizara ya maji.

Aidha, Mhe. Aweso anasisitiza kwamba kada zote zilizopo ndani ya wizara ya maji zifanyekazi kwa kushirikiana ili kuendelea kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dr Samia Suluhu Hassan dhamira yake ya kumtua ndoo mama kichwani.

Akizungumzia utendajikazi wa Maafisa Utumishi na Rasilimali Watu, Mhe. Aweso anawaasa Maafisa Utumishi hao kufanyakazi kwa weledi, haki na kutafsiri vizuri sheria na kanuni za kiutumishi.

Maeneo mengine ambayo anawaelekeza Maafisa Utumishi hao ni kuwajengea mazingira mazuri watumishi, kushughulikia changamoto za watumishi kwa haraka, kuacha kuwatisha watumishi, kutoa stahiki za watumishi kwa haki,kufanya vikao na watumishi pamoja na kujenga uhusiano mzuri na watumishi.

Akihitimisha hotuba yake, Mhe. Aweso anawashukuru watumishi wote ndani ya wizara ya maji kwa kuendelea kuiheshimisha wizara ya maji. Anasena kwamba mafanikio haya mazuri yamesababishwa na utendajikazi mzuri wa kila mtumishi wa wizara ya maji na kwamba akiwa Waziri mwenye dhamana kubwa ndani ya wizara ya maji ataendelea kutoa ushirikiano wake kuhakikisha kwamba wizara ya maji inaendelea kuwa mfano mzuri kwa wizara zingine hapa nchini.

Mkutano huu ambao umewaleta pamoja kada za Habari, Utumishi na Maendeleo ya Jamii ni wa kwanza kufanyika tangu Mhe. Aweso ateuliwe kuwa Waziri wa Maji na umeshehereshwa na Mhe. Aweso kwa kuagiza kwamba mkutano huu uwe endelevu na ufanyike kila mwaka.