ELIMU YA UTUNZAJI WA CHANZO CHA MAJI YA ZIWA VICTORIA-IHELELE SASA YAZIFIKIA SHULE ZA SEKONDARY NA MSINGI
Katika kupanua wigo wa utoaji wa elimu ya utunzaji wa chanzo cha maji ya Ziwa Viktoria huko Ihelele Misungwi - Mwanza inayotolewa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama Shinyanga (KASHWASA) sasa imezifikia shule za sekondari na msingi zilizopo jirani na chanzo hicho cha maji.
Akizungumza mapema leo tarehe 30/10/2024 huko Mbarika Misungwi kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa KASHWASA, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa KASHWASA Dkt. Mwidima Peter anasema kwamba lengo la kufikisha elimu hiyo ya utunzaji wa chanzo hicho cha maji kwenye shule za sekondari na msingi ni kuongeza wigo wa utoaji huo wa elimu ya uhifadhi na utunzaji wa chanzo hicho muhimu cha maji.
Dkt. Mwidima anaelezea kwamba awali elimu hiyo ilikuwa ikitolewa kwa viongozi wa kata, vijiji na kwa wananchi kupitia mikutano ya ndani na ya hadhara lakini kwa kutambua mchango na nguvu kubwa waliyonayo vijana kwenye jamii KASHWASA imeamua kufikisha elimu hiyo kwa vijana hao kwa lengo la kupata mabalozi wengi watakaosaidia kusambaza elimu hiyo ya Mazingira kwa familia na jamii wanazotoka.
Utoaji huo wa elimu ambao ni endelevu mbali na kuwafikia wanafunzi wa shule za sekondari na msingi unaenda sambamba na mikutano ya hadhara kwenye kata zote tano zilizopo kwenye mwambao mwa chanzo cha maji cha Ihelele upande wa Misungwi-Mwanza. Kata hizo ni Kasololo, Sumbugu, Mbarika, Ilujamate na Lubili