WASIOJULIKANA WAHUJUMU MIUNDOMBINU YA MAJI YA KASHWASA, WAANZISHA KILIMO CHA BUSTANI
Watu wasiojulikana wamefanya uharibifu wa miundombinu ya maji ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama Shinyanga (KASHWASA) na kuanzisha kilimo cha bustani.
Hali hiyo imebainishwa jana tarehe 29/10/2024 na Meneja wa Huduma kwa Wateja wa KASHWASA Ndugu John Zengo Ngano alipokuwa akitoa taarifa hizo kwa Menejimenti ya KASHWASA Mjini Shinyanga.
Ndugu Zengo anasema kwamba alipokea taarifa za uwepo wa hujuma hizo kutoka kwa mwananchi mwema na mara baaya ya kupokea taarifa hizo alielekea eneo la tukio na kukuta uwepo wa kilimo hicho cha bustani ambacho kinatumia maji ya KASHWASA ambayo wahusika hao wanayapata baada ya kuvunja Airvalve na kusababisha maji kuwa yanamwagika kwa wingi na wao kutumia maji hayo kwenye shughuli hiyo ya kilimo cha mbogamboga.
Aidha, Ndugu Zengo anasema kwamba hawakufanikiwa kukamata mtu yoyote baada ya wahusika wa uharibifu huo kukimbia. Hata hivyo Meneja huyo wa Huduma kwa wateja anasema tayari Ofisi yake imeshafungua kesi kwenye kituo cha Polisi cha Maganzo na kupewa RB namba MGZ/RB/700/2024 ambapo watuhumiwa wanaendelea kutafutwa na jeshi la polisi.
Tukio hili ni muendelezo wa matukio mengine ya uharibifu na hujuma ambayo yamekuwa yakifanywa kwenye miundombinu ya maji ya KASHWASA na hivyo kusababisha ongezeko kubwa la upotevu wa maji pamoja na kufifisha uhakika wa upatikanaji wa maji kwa wateja wanaohudumiwa na KASHWASA.