Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya KUWASA Bi.Stewart Bulaya akizungumza na Watumishi wa KASHWASA katika Ukumbi wa Mkutano wa KASHWASA uliopo Ihelele-Misungwi,Mwanza.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya KASHWASA Dr. Edith Kwezi (aliyesimama kulia) akizungumza wakati wa Ziara hiyo.
KASHWASA YABEBA MATUMAINI YA WENGI .
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama Shinyanga imebeba matumaini ya Wananchi wengi wakiwemo wateja wa Mamlaka hiyo ya maji ambao wanategemea Chanzo cha Uzalishaji Maji Ihelele,Wilaya ya Misungwi Mkoa wa Mwanza.
Hali hiyo imejidhihirisha jana tarehe 21 Oktoba 2024 katika Ziara ya Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama (KUWASA).
Akizungumzia hali hiyo ya matumaini iliyobebwa na KASHWASA, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya KUWASA Bi. Stewart Bulaya anasema kwamba KASHWASA inategemewa na ni tumaini kubwa sana kwa wateja na wananchi ambao wanategemea maji kutoka Ziwa Viktoria na hawana chanzo kingine cha Maji zaidi ya maji hayo.
Mwenyekiti huyo wa Bodi ameongeza kuwa maelfu ya Watanzania wanatumia maji ya KASHWASA katika shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na viwanda ambavyo vinachochea maendeleo ya kiuchumi katika nchi yetu na hivyo kuifanya KASHWASA kuwa tumaini na tegemeo kubwa kwenye shughuli hizo za kiuchumi.
Aidha,Mwenyekiti Bodi ya KUWASA ameonyesha kuridhishwa na jitihada za KASHWASA katika kuhakikisha shughuli za Uzalishaji Maji zinaendelea licha ya changamoto ya madeni kutoka kwa wateja wake.
KASHWASA kwa sasa inahudumia Mikoa sita ya Geita, Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Tabora na Singida ambapo mtandao wake wa maji kwenye Bomba kubwa ni zaidi ya KM 807.